Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) kwa kushirikiana na Global Peace Foundation imeandaa mdahalo muhimu uliowakutanisha viongozi wa dini, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, taasisi za serikali na zisizo za serikali, pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii ili kujadili amani na siasa safi kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao (2025).
Sheikh Dkt. Al-Hadi Mussa Salum, Mwenyekiti wa JMAT-TAIFA, amesema kuwa mdahalo huu ni sehemu ya utekelezaji wa katiba ya jumuiya hiyo ambayo inalenga kusimamia maridhiano, mshikamano wa kitaifa na kulinda amani bila kujali dini, mila, rangi au itikadi za kisiasa.
Amesisitiza kuwa uchaguzi ni fursa ya kuonyesha uzalendo wa kitaifa na njia ya Amani ya kuchagua viongozi wa Taifa kwa heshima na uwazi.
Mdahalo huu ulihudhuriwa na viongozi wa dini mbalimbali, vyama vya siasa, vyombo vya habari, wanawake, watu wenye ulemavu pamoja na taasisi za kijamii na serikali.
Maudhui na Lengo Kuu la Mdahalo
Sheikh Dkt. Al-Hadi Mussa Salum amesema kuwa lengo kuu la mdahalo huo ni:
- Kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa haki, amani na uwazi katika uchaguzi.
- Kupunguza mvutano wa kisiasa na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
- Kusisitiza heshima kati ya wagombea na wapiga kura.
- Kuhimiza tume ya uchaguzi, vyombo vya usalama na mahakama kufanya kazi kwa uadilifu na usawa.
Wito kwa Vyombo vya Habari
Mwenyekiti wa JMAT aliwataka waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kusimamia maadili ya taaluma yao kwa kuripoti kwa uaminifu, kuchunguza taarifa kabla ya kuzitoa, na kupinga upotoshaji. Pia aliwataka kutoa jukwaa la wazi kwa majadiliano ya sera za wagombea.
Your Comment